Ijumaa 30 Januari 2026 - 01:00
Ajenda ya Marekani na Wazayuni dhidi ya waandishi wa habari wa Lebanon; kuanzia kuitwa mahakamani wakurugenzi wa vyombo vya habari vinavyounga mkono Muqawama hadi kuuawa waandishi wa habari

Hawza/ Wanahabari na waandishi wa habari wa Lebanon wanaounga mkono Muqawama katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wamekuwa chini ya shinikizo la kisiasa, kufuatiliwa kisheria bila sababu halali, na hatimaye kuuliwa kwa makusudi na utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, waandishi wa habari wa Lebanon wanaouunga mkono Muqawama katika mwaka uliopita, kama ilivyo kwa makundi mengine ya jamii ya Lebanon yanayounga mkono uhuru na mamlaka ya nchi yao na kupinga kuhalalisha uhusiano na utawala haram, wamekuwa wakilengwa na mashambulizi, manyanyaso na mateso kutoka ndani na nje ya Lebanon.

Wanahabari wanaouunga mkono Muqawama nchini Lebanon, kwa sababu tu ya kusimama upande wa mamlaka  huru ya kisiasa ya Lebanon na kupinga mashambulizi na hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya uadilifu wa ardhi ya Lebanon, wamekabiliwa na kuitwa kutoa maelezo, kuhojiwa na kufuatiliwa kisheria.

Shahidi Sheikh Ali Nouruddin, mwandishi wa habari wa Lebanon, aliuawa kishahidi katika shambulio la hivi karibuni la kigaidi lililotekelezwa na utawala wa Kizayuni. Hezbollah ya Lebanon katika taarifa yake ilitoa rambirambi kwa kuuwawa kishahidi kwa mwandishi huyo wa habari wa Lebanon na ikasisitiza: “Kulengwa mwandishi wa habari shahidi Sheikh Ali Nouruddin kunaonesha hatari ya mashambulizi endelevu ya adui dhidi ya vyombo vya habari kwa aina na majina yake yote; jambo hili ni muendelezo wa sera ya mauaji ya kimfumo na jitihada za kuzima sauti ya ukweli na sauti huru.”
Katika taarifa hiyo, wanahabari wote, Wizara ya Habari, taasisi za habari, vyama, taasisi pamoja na watu binafsi wa kisiasa na kiakili wametakiwa kuchukua hatua katika majukwaa yote ya ndani, ya Kiarabu na ya kimataifa, hususan katika taasisi za haki za binadamu, za kisheria na za kibinadamu, ili kudhibiti ukatili huu wa Kizayuni na kuinua sauti zao.

Katika muktadha huohuo, Zulfiqar Zaher, mwandishi wa Lebanon, ameandika makala ifuatayo: Katika nchi ambayo hapo awali ilijivunia uhuru, ulinzi wa uhuru wa kujieleza na kuwaacha wananchi watoe maoni yao bila vikwazo — hadi pale Rais marehemu Salim al-Hoss aliposema wakati mmoja: “Nchini Lebanon kuna uhuru mwingi na demokrasia ndogo” — leo hii uhuru wa kujieleza upo hatarini. Tunashuhudia manyanyaso na kuitwa kwa viongozi wa fikra, waandishi wa habari na sura za vyombo vya habari, kwa sababu tu wametoa maoni na uchambuzi wa kisiasa kuhusu masuala yanayowahusu wananchi, yanayohusiana na haki halali ya kujilinda dhidi ya adui wa Kizayuni, au yanayohusiana na utendaji wa mamlaka ya kisiasa na kushindwa kwake kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda Wale­banon dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel.

Yanayotokea yanaibua maswali kuhusu utendaji wa vyombo vya usalama na mahakama, ambavyo katika matukio mengi ya majaribio ya kumkaribia adui au kutaka kuanzishwa uhusiano au kuhalalishwa mahusiano nayo, havikuchukua hatua yoyote; hadi kufikia hatua ambapo baadhi yao wanahalalisha uvamizi wa Kizayuni dhidi ya makundi au maeneo fulani ya Lebanon.

Hali hii inazua maswali mengi: Je, kuitwa waandishi wa habari mbele ya mahakama za jinai kisheria kunaruhusiwa, au mamlaka husika ni Mahakama ya Vyombo vya Habari? Je, wito huu una uhalali wa kisheria, au una misukumo ya kisiasa ya kulipiza kisasi, au unawalenga watu au upande maalumu? Na vipi kuhusu kila mwandishi wa habari anayenyanyua sauti yake kupinga uvamizi wa Israel, ikilinganishwa na wale wanaonyamaza au hata kuutetea?

Je, katika siku za nyuma, kumkosoa Rais — awe ni rais wa sasa au waliomtangulia kama Rais Michel Aoun na Rais Émile Lahoud — halikuwa jambo la kawaida? Kwa nini basi hakuna aliewahi kuwawajibisha waliokuwa wakizungumza dhidi ya Rais au wanasiasa wengine? Kwa nini vyombo vya usalama na mahakama havikuchukua hatua? Kwa nini leo kunafanyika mashambulizi makali dhidi ya yeyote anayemkosoa Rais au 

mtu mwingine yeyote? Je, lengo ni kuigeuza nchi kuwa “dola ya kipolisi” ili kukabiliana na yeyote anayepinga maoni ya watu au taasisi fulani?

Na vipi kuhusu uhuru wa kujieleza ambao unahakikishwa na sheria na Katiba ya Lebanon? Kwa nini kuna viwango viwili? Baadhi wanaona ni haki yao kutoa maoni yao, hususan kuhusu uhusiano na adui, wito wa kuhalalisha uhusiano naye, na hata kumchochea adui kuwaua wananchi wa Lebanon; lakini leo, taasisi fulani za kisiasa, kisheria na za habari hukasirika sana pale taasisi ya kisiasa inapokosolewa.

Je, kinachofanyika ni utetezi wa mamlaka ya kitaifa na sheria, au ni utetezi wa wale wanaofanya uzembe na wanaoogopa kukabiliana na mvamizi? Na walinzi wa mamlaka ya taifa dhidi ya mashambulizi ya kila siku ya Israel dhidi ya Lebanon kwa mwaka mzima hadi leo wako wapi?

Kuhusu masuala haya yote, Randali Jabbour, rais wa Muungano wa Vyombo vya Habari vya Sauti na Picha nchini Lebanon, alisema: “Ni wazi kwamba wito huu ni kinyume cha sheria na una motisha za kisiasa, na unalenga kuzima sauti zinazoipinga Israel na kuwafichua baadhi ya maafisa wanaowekwa chini ya shinikizo au wanaotekeleza ajenda ya Kimarekani–Kizayuni.”
Aliongeza: “Uhuru na haki zina mipaka yake; la sivyo kwa nini ni wale walio upande mmoja tu wanaoitwa, ilhali wale walio upande wa kupinga Muqawama wanawashambulia viongozi wake na hata wafuasi wake bila yeyote kuwaambia chochote?”

Jabbour, katika mahojiano maalumu na tovuti ya televisheni ya Al-Manar, alisema: “Lengo ni kuzima sauti za Muqawama, kukandamiza wanaompinga Israel, na kuongeza shinikizo kwa yeyote anayepinga kuhalalisha uhusiano, ili kurahisisha utekelezaji wa mradi wa Kimarekani–Kizayuni.”
Alibainisha kuwa “katika kipindi cha urais wa Émile Lahoud na Michel Aoun, kulifanyika ukiukwaji mwingi, hata kufikia kuandaliwa kwa kampeni kama ‘Falah’ na nyinginezo, na kutokea kwa ‘Mapinduzi ya Halla’, lakini hakuna aliyechukua hatua.”
Alifafanua kuwa “marais hawa wawili walikuwa wavumilivu sana na hawakutumia ukandamizaji, na pili, kwa sababu ya mkondo wa kisiasa walioufuata; hivyo, wale wanaodai leo kuwa watetezi wa urais, ndio haohao waliokuwa wakiuchezea na kuudhoofisha hapo awali.”

Jabbour alisema pia: “Dunia nzima imegeuka kuwa dola ya kipolisi; na yeyote anayepinga Marekani hulengwa, hata ndani ya Marekani yenyewe inayojigamba kwa uhuru na kuinua bendera yake kwa juu juu.”
Alisisitiza kuwa wale wanaodai kulinda mamlaka ya kitaifa wako mbali sana nayo, na mamlaka yao ni sera dhidi ya Muqawama tu. Hawatikiswi na mashambulizi ya Israel; bali wanayatia moyo ili kuangamiza sehemu ya wananchi wa Lebanon.

Kwa upande wake, Rami Bou Melhem, mtafiti wa sheria na wakili, alisema: “Sheria haitathaminiwa kwa umbo lake tu, bali kwa vigezo vyake. Wito wa kuitwa unaweza kutolewa kwa sura ya kisheria, lakini pale mwandishi wa habari anapofuatiliwa kwa sababu ya maoni ya kisiasa ya kiuchambuzi, ilhali kauli na uchochezi mzito zaidi na wa wazi wa kihalifu unaachwa bila kushughulikiwa, basi ni lazima kuhoji motisha halali za msingi.”
Aliongeza: “Tatizo si wito wenyewe, bali ni ubaguzi, wakati na vigezo vyake; jambo hili huzua wasiwasi kuhusu kuwepo kwa motisha za kisiasa badala ya za kisheria.”

Bou Melhem, katika mahojiano maalumu na tovuti ya televisheni ya Al-Manar, alisisitiza kuwa: “Katiba ya Lebanon, hususan Ibara ya 13, iko wazi na bayana katika kulinda uhuru wa maoni na kujieleza. Hii si fadhila ya mtu yeyote, bali ni haki ya msingi.”
Alifafanua kuwa “tatizo la leo si katika matini zenyewe, bali katika kuwekewa mipaka tafsiri zake,” na akaongeza: “Uhuru wa kujieleza haupimwi pale maoni yanapokuwa mepesi kwa mamlaka, bali hupimwa pale yanapokuwa ya ukosoaji na makali; na njia yoyote inayozuia haki hii hupiga pigo kwenye moyo wa nchi ya kidemokrasia.”

Wakili Bou Melhem alisema: “Tunakabiliwa na mgongano wa wazi na Katiba, na Sheria ya Vyombo vya Habari inayotofautisha kati ya maoni ya kisiasa na kashfa, pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa ambao Lebanon ni miongoni mwa nchi zilizosaini.”

Alieleza kuwa “maoni ya kisiasa, hata yawe makali kiasi gani, hayawi kosa la jinai isipokuwa yawe na matusi binafsi au uchochezi wa moja kwa moja. Kupanua kanuni za jinai ili kujumuisha uchambuzi wa kisiasa ni tafsiri ya kiholela inayokiuka misingi ya haki.”

Akizungumzia vitendo vya kiholela vya vyombo vya usalama na mahakama na matumizi yao ya viwango viwili, Bou Melhem alisema: “Ukweli unaongea wenyewe, au angalau unaibua taswira hatari. Tunapoona hatua za haraka zikichukuliwa dhidi ya maoni fulani, ilhali tunanyamaza kabisa mbele ya uchochezi wa kikabila au uhalalishaji wa uvamizi wa Israel, basi tunakabiliwa na kiwango cha wazi cha viwango viwili katika utekelezaji wa sheria.”
Alisisitiza: “Haki, ikiwa haitatekelezwa kwa kipimo kimoja kwa wote, basi si haki.”

Bou Melhem alisema pia: “Marais wa zamani walikabiliwa na ukosoaji wa moja kwa moja na mkali, wakati mwingine mkali zaidi kuliko tunachosikia leo, na wakati huo hakuna kesi wala wito kama huu uliofunguliwa.”
Akaendelea: “Swali lililo wazi ni: nini kilichobadilika? Je, sheria imebadilika? Au namna ya kuitumia? Au je, maudhui ya maoni ya kisiasa yamekuwa kipimo badala ya msingi wa kisheria?”

Aliongeza kwa kusema: “Swali la msingi ni hili: je, sheria zinatumiwa kuwafuatilia wale wanaokataa uvamizi wa Israel na kuinua sauti zao katika kutetea mamlaka na heshima ya kitaifa, ilhali macho yanafungwa kwa wale wanaohalalisha uvamizi huo au kuupa mwavuli wa kisiasa na wa habari?”
Aliendelea kuwa: “Ikiwa hii ndiyo njia, basi tunakabiliwa na dosari kubwa katika vipaumbele vya kisheria, jambo linalotishia amani ya kijamii na kudhoofisha imani kwa dola.”

Bou Melhem alihitimisha kwa kusisitiza: “Tunatetea mahakama huru na yenye nguvu, na utekelezaji wa sheria kwa wote bila ubaguzi. Hata hivyo, tunapinga kwa nguvu yoyote ile mbinu ya kibaguzi inayozuia uhuru na kuipokonya Katiba kiini chake. Haki haigawanyiki, na uhuru wa kujieleza si upendeleo unaotolewa kwa baadhi na kunyimwa wengine.”

Ikumbukwe kwamba waandishi wa habari wanaonyanyaswa leo ndio watetezi wa kweli wa mamlaka ya kitaifa na wa muqawama dhidi ya ukaliaji wa Israel na uvamizi wake endelevu dhidi ya mamlaka ya Lebanon. Hawako tayari kuficha vichwa vyao kwenye mchanga na kupuuza ukiukwaji wote unaotokea. Kwa hiyo, manyanyaso haya yote yanafanyika katika muktadha wa vita endelevu dhidi ya Muqawama na mazingira yake ya uungaji mkono, ambayo ndiyo chanzo cha nguvu ya Lebanon.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha